Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa Shirika la wanyamapori nchini KWS, Dkt Richard Leakey amejitokeza kukanusha madai kwamba filamu inayoitwa 'Africa' inayolenga kuangazia maisha yake itaandaliwa nchini Afrika Kusini.

Kupitia kwa taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Alhamisi, Leakey alitupilia mbali taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye gazeti moja la humu nchini siku ya Jumanne.

Alisema amekuwa akizungumza mara kwa mara na waandalizi wa filamu hiyo, na kwamba hajapokea taarifa yoyote kuhusiana na uandalizi wa filamu hiyo kuhamishwa hadi nchini Afrika Kusini.

Aidha, alisema kuwa majadiliano yangali yanaendelea na kuongezea kuwa ana amini kwamba lengo lingalipo la kuandaa filamu hiyo hapa nchini.

Hata hivyo, Leakey katika taarifa yake alisisisitiza kuwa ni lazima filamu hiyo iandaliwe hapa nchini kwani maisha yake yamekuwa hapa Kenya.

Taarifa iliyokuwa imeandikwa kwenye gazeti alisema kuwa mtayarishaji wa filamu hiyo Richard Harding alisema filamu hiyo itahamishwa kutoka hapa nchini hadi nchini Afrika Kusini, kwa kuwa Kenya haina soko lenye faida kwa filamu zinazotengezwa hapa nchini.

Filamu hiyo ya Afrika inayoangazia maisha ya mwana mazingira huyo inaongozwa na mwigizaji maarufu wa Hollywood Angelina Jolie.