Wabunge wa muungano wa Jubilee wamesema kuwa wataendelea kupigana dhidi ya jinamizi la ufisadi ambalo amesema linatishia kuwapotezea imani ya wapiga kura.
Kupitia kwa mbunge mmoja wa muungano huo, Mithika Linturi ambaye anawakilisha eneo bunge la Igembe South, kwenye kikao na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika mkahawa mmoja mjini Mombasa, wabunge hao walisema kuwa jukumu lao kama wabunge ni kuendeleza vita vikali dhidi ya ufisadi.
Alisema kuwa wanaelewa ugumu ulioko na wako tayari kurudisha imani ya wakenya na kuwaomba wananchi kujiunga na juhudi hizo kwa kuhakikisha kuwa wanatoa ripoti za ufisadi kwenye idara.
“Tutaendelea kusukuma na kushinikiza vita dhidi ya wafisadi na ufisadi. Wabunge, mafisaa wa serikali, kila mkazi na wananchi wenye nia safi ni hsarti tusimama upande wa mbele kusaidia katika kuliangamiza jinamizi hili la ufisadi, hivyo tukae macho na kutoa ripoti za ufisadi,” alisema Linturi.
Haya yanajiri huku kitandawili cha kung’atuka kwa waziri wa ugatuzi kikiendelea, huku baadhi ya wabunge kutoka serikali ya Jubilee wakiendelea kumtaka aondoke ili uchunguzi kufanyika.
Upande wa upinzani nao umeahidi kufanya kila juhudi kuona waziri huyo anaondolewa ofisini na kudokeza kuwa wataunga mkono mswada ambao unaoletwa bungeni na Mbunge Alfred Keter.