Wamiliki wa matatu, abiria na wahudumu katika sekta ya magari ya masafa marefu pamoja na mashirika ya utetezi wa haki za binadamu watahitajika kutuma malalamishi yao kuhusu maafisa wa trafiki na polisi wa kitengo cha ujasusi.
Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatatu mjini Mombasa wakati wa kuhamasisha polisi kuhusu ukaguzi huo, kamishna katika tume ya huduma kwa polisi Murshid Mohamed alisema wanalenga kuwakagua maafisa wa polisi 12,000 Kenya nzima.
Aidha, alieleza kwamba afisa yeyote asiyetaka kukaguliwa basi hatakuwa na budi ila kujiuzulu.
Katika ukaguzi huo, tume hiyo itazingatia kiwango cha elimu, taaluma, maadili na haki za binadamu, vile vile watahitaji taarifa za benki za maafisa hao, na taarifa za mali zao.
Maafisa watakaopatikana na makosa madogo ya ufisadi watapewa adhabu na wale wenye makosa makubwa wataachishwa kazi.