Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya maafisa tawala kupewa pikipiki kusaidia kuimarisha usalama katika kaunti ya Mombasa, sasa wakaazi wa eneo la Kisauni, Jomvu, Changamwe na Likoni wanataka maafisa hao kutekeleza jukumu lao vyema.

Wakaazi hao wamesema kuwa kwa muda usalama wa maeneo hayo umekumbwa na changamoto na iwapo maafisa hao tawala watatumia pikipiki hizo kuunganisha jamii basi kwa kiwango kikubwa usalama wa kaunti ya Mombasa utaimarishwa.

Wakiongozwa na Charles Mngane, wakaazi hao wamewataka maafisa hao tawala waliyopokea pikipiki hizo kuhakikisha kuwa wanaenda mikutano ya baraza la kiusalama ili kuona kwamba suala la usalama linatekelezwa na jamii yote kwa jumla.

“Tunawataka maafisa hao tawala kutumia pikipiki hizo kutembelea wakaazi hata wa mashinani kuhakikisha kuwa wanajadiliana nao vyema na kufanya mikutano ya baraza na kusaidia kusitisha visa vya kihalifu,” alisema Mngane siku ya Ijumaa katika eneo la Changamwe wakati wa mkutano wa kiusalama.

Mngane amesisitiza kuwa usalama wa kaunti ya Mombasa utaimarika zaidi kwa ushirikiano wa maafisa tawala, viongozi wa kaunti hiyo, wakaazi na maafisa wa usalama huku akiwahimiza wakaazi kuwa katika mstari wa mbele kutoa habari muhimu kuhusu washukiwa wa uhalifu na kutiwa nguvuni.

Pendekezo la wakaazi hao limejiri siku moja tu baada ya maafisa tawala kupokea pikipiki watakazotumia kusaidiana na wakaazi wa kaunti ya Mombasa kuimarisha usalama.