Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Maafisa wa polisi wa eneo la Gilgil kwenye kaunti ya Nakuru wamekanusha madai ya kupata mwili uliokuwa ukioza katika eneo la kupimia uzani wa magari (Gilgil Weighbridge) siku ya Alhamisi.

Kupitia kwa mahojiano kwa njia ya simu, OCPD wa Gilgil Serah Koki alisema hawana taarifa yoyote kuhusiana na mwili unaodaiwa kupatikana katika eneo lile.

Ni matamshi ambayo ameyatoa baada ya ripoti kusambaa, jijini Nakuru zikiashiria kwamba mmoja wa wafanyibiashara wawili waliotoweka siku sita zilizopita alipatikana akiwa ameuwawa katika eneo hilo.

Hata hivyo, amekariri kwamba makachero kutoka kwa kitengo cha polisi cha divisheni ya Bahati wanafanya uchunguzi kuhusiana na Jamaa hao wawili waliotoweka.

Inaarifiwa kwamba wafanyibiashara hao wawili walitekwa nyara na watu waliokuwa na bunduki mwendo wa saa tano mchana Ijumaa ya tarehe 22 Januari mwaka huu na wanamme wane katika eneo la Whitehouse viungani mwa mji wa Nakuru.

Siku ya Jumatano wiki iliyopita, familia za wafanyibiashara hao wawili waliotoweka zilihimiza maafisa wa polisi kuongeza kasi katika shughuli ya kuwatafuta wawili hao, wakilalama kwamba maafisa wa polisi walikuwa wakijiburura katika uchunguzi wao.

Wafanyibiashara hao wawili ambao pia walikuwa viongozi wa sekta ya usafiri wa umma mjini Nakuru wanafahamika kama Joseph Ngugi Chege almarufu Jose na Simon Wachira almaarufu Shem .

Hata hivyo, kamanda wa Kaunti ya Nakuru Hassan Barua aliyezungumza na wanahabari hapo siku ya Jumatano ya tarehe 27 Januari kwa njia ya simu alikanusha madai kwamba maafisa wa polisi wanajikokota katika uchunguzi wao wa kuwatafuta wawili hao akisema uchunguzi huo ungali unaendelea.