Bunge la Kaunti ya Nyamira limeanza kuwachunguza upya mawaziri wanne na makatibu wawili wa wizara mbalimbali ambao walikuwa wamehusishwa na madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.
Wakihutubu kwenye kikao katika mkahawa mmoja kule Kisumu siku ya Alhamisi wanachama wa kamati ya uhasibu wa pesa za umma kwenye bunge la kaunti ya Nyamira walisema kuwa wamelazimika kuanzisha upya uchunguzi huo ili kubaini jinsi pesa za umma kwenye idara mbalimbali za serikali ya kaunti hiyo zilizovyo tumika.
"Tumeamua kuanza kuwapiga upya msasa mawaziri wanne na makatibu wawili kwenye wizara mbalimbali kwa kuwa tunataka kubaini ukweli na ni vipi pesa zilizotengewa miradi mbalimbali kwenye mwaka wa kifedha wa 2013/2014 zilivyo tumika," alisema naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Zipporah Osoro.
Mwenyekiti wa kamati ya uhasibu wa pesa za umma Ezra Mochiemo alisema kuwa kamati yake imechukua hatua hiyo yakuwachunguza upya maafisa husika baada ya wananchi kuzua tetezi kuwa kamati iliyoteuliwa hapo awali ili kuwachunguza mawaziri na makatibu hao ilikuwa na mapendeleo kwenye mapendekezo yao.
"Kwa kweli wakazi wengi wa kaunti ya Nyamira wamekuwa wakizua tetezi kuwa kamati teule ya bunge iliyokuwa na wanachama sita, iliyopewa majukumu yakuchunguza maafisa husika kuhusiana na tuhuma za ufisadi ilidhihirisha mapendeleo kwenye uchunguzi wao, na ndio maana tumeanzisha uchunguzi upya il kubaini iwapo mawaziri hao wanne na makatibu wawili wanahusika na tuhuma za ufisadi," alisema Mochiemo.
Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama alilazimika kuwarejesha mawaziri hao na makatibu wawili kazini baada ya bunge la kaunti ya Nyamira kutupulia mbali ripoti ya kamati teule iliyowapata na hatia mawaziri wawili nakuwasaza wengine.