Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kamanda mkuu wa polisi kaunti ya Mombasa Francis Wanjohi amepinga madai yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa kuwa maafisa wa polisi wanawadhulumu wakazi kwa kuwatia nguvuni bila hatia katika oparesheni ya kiusalama kaunti hiyo.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Wanjohi alisema kwamba kamwe maafisa wa polisi hawajawakamatwa wakazi kiholela wala kuwadhulumu haki zao, bali wanazingatia sheria na akasema kwamba lazima wakazi wa kaunti hiyo kuwa salama.

Kulingana na Wanjohi, operesheni zinazotekelezwa na maafisa wa polisi huanzia saa nne za usiku na wala sio saa moja jioni kama wanavyodai viongozi hao wa kisiasa, na akawata viongozi hao kutoliingiza siasa swala la usalama kwani huenda hatua hiyo ikazua taharuki.

Wanjohi aidha amewataka wakazi kushirikiana kwa karibu mno na maafisa wa polisi katika kuimarisha usalama wa kaunti hiyo ili kuwawezesha maafisa hao kuwapa wakazi ulinzi dhabiti na kuzuia kuchipuka kwa visa vya kihalifu.

"Tunaomba viongozi wa kisiasa kukoma kuingiza siasa swala la usalama kwani maafisa wa polisi wanatekeleza jukumu lao kisheria, na tunawashinikiza wakazi kushirikiana na maafisa wa polisi ili kuimarisha usalama," alisema Wanjohi.

Kauli ya Kamanda huyo mkuu wa polisi imejiri siku chache tu baada ya Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharrif Nassir kusema kwamba ataongoza maandamano makubwa mjini Mombasa kupinga operesheni ya kiusalama inayotekelezwa na maafisa hao kwani inakiuka haki za jamii.