Maafisa wa polisi katika eneo la Likoni mjini Mombasa wanamsaka kijana mmoja wa miaka 21 anayedaiwa kumlawiti binamu yake wa miaka saba.
Kulingana na Maafisa hao, Mvulana huyo anayefahamika kama Shaffi Minyi Salim alimlawiti mtoto huyo mdogo wa kiume katika mtaa wa Majengo eneo bunge la Likoni mjini Mombasa siku ya Ijumaa.
Maafisa hao wamesema kwamba kijana huyo huenda ameenda mafichoni baada ya kutekeleza uovu huo na msako mkali dhidi yake ungali unaendelea ili kumtia nguvuni.
Akiongea na wanahabari afisini mwake katika kituo cha polisi cha Likoni mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Afisa Mkuu wa Polisi wa eneo la Likoni Willy Simba alikiri kupokea taarifa hizo za ubakaji na kushikilia kwamba uchunguzi unaendelea ili kumtia nguvuni mshukiwa.
“Tumepokea taarifa hizo za ubakaji na maafisa wangu wa polisi wameanzisha uchunguzi kumsaka mshukiwa huyo," alismema Bw Simba.
Katika siku za hivi majuzi, visa vya ubakaji vimeripotiwa kukithiri mno katika eneo hilo la Likoni na kaunti nzima ya Mombasa.