Shirika la bandari nchini siku ya Jumanne lilitambulisha usimamizi mpya kwa wafanyakazi wengine na kuanza majukumu yao rasmi huku wakitakiwa kuwajibika zaidi na kutenda kazi yao bila kuingiliwa na ushawishi wowote.
Usimamaizi huo mpya umeombwa kutumia uwezo wao na kufanikisha malengo ya shirika hilo bila kuvunja sheria kwa namna yoyote ile.
Akiongea kwenye hafla hiyo ya kuwatambulisha maafisa wakuu hao, mwenyekiti wa kamati simamizi ya bandari hiyo meja mstaafu Marsden Madoka alisema kuwa shirika hilo sasa litafanya kazi yake kwa kufuata utaratibu uliopo, na kuweka wazi kuwa bado wataendelea kupigana na masuala yoyote ambayo yanaleta utata bandarini .
Wakiandamana na mkurugenzi Catherine Mturi-Wairi, ambaye ameteuliwa kuwa kaimu meneja mkuu wa shirika hilo, Madoka ameomba ushirikiano baina ya wafanyakazi wa shirika hilo pamoja na maafisa hao wakuu wapya.
Shirika hilo la bandari linaendelea kufanya juhudi za kusafisha maovu na visa vya ufisadi ambavyo vimekuwa vikichipuka, ambapo tayari maafisa zaidi ya wanane wakuu wa shirika walisimamishwa kazi na wengine kutumwa kwenye likizo ya lazima.
Hatua hiyo ya kamati simamizi ya bandari imeweza kupata uungwaji mkono kutoka kwa wakazi pamoja na viongozi wa kisiasa katika eneo zima la pwani.
Mwenyekiti wa bodi ya shirika la bandari nchini Marsden Madoka kwenye kikao ofisini. Kamati mpya ya kuchukua usukani imeteuliwa