Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi amepongezwa kwa kuongoza viongozi wa eneo la Kisii hadi Eldoret kwa Naibu Rais William Ruto ili kuleta maendeleo katika eneo hilo, maendeleo ambayo yameonekana kuwa nyuma kwa wakati mrefu ikilinganishwa na sehemu zingine za nchi.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi mjini Kisii, muungano wa vijana kutoka eneo bunge la Bonchari kwa jina ‘Kisii Youth convention’ wakiongozwa na mwenyekiti wao Douglas Okari walimpongeza Maangi na kusema kuwa sasa maendeleo yataonekana katika kaunti hiyo.

“Sisi wenyewe tulikuwa miongoni mwa wale walienda kwa naibu Rais William Ruto wiki jana na tuliyoyazungumzia ni maendeleo na sio siasa na tunatarajia maendeleo kuanza kufanyika katika kaunti ya Kisii,” alisema Okari.

“Tunapongeza Naibu Gavana wetu wa Kisii Joash Maangi kwa kutuongoza kwani tulienda kuleta maendeleo katika Kaunti ya Kisii wala sio misingi ya kisiasa,” aliongeza Okari.

Wakati huo huo, John Mokaya, mwanachama wa muungano huo wa vijana alisema kiongozi yeyote hawezi kufuata chama cha kisiasa ila tu kuleta maendeleo .

Hayo yalijiri baada ya Maangi, ambaye ni katibu wa chama cha ODM katika Kaunti ya Kisii kukosolewa kwa kukutana na viongozi wa Jubilee na kusemekana kusaliti chama chake, huku Maangi akikana hayo na kusema anataka maendeleo na sio siasa za vyama.