Naibu Gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi amewashauri wanasiasa kujitenga na siasa za uchaguzi ujao na kufanya maendeleo kwanza.
Kulingana na Maangi, sharti viongozi kuheshimiana miongoni mwao na kukumbatia umoja na kufanya maendeleo kwa ajili ya mwananchi na kuacha matamshi ambayo si ya kujenga nchi kwa kukosoa wengine.
Akizungumza mnamo siku ya Jumanne mjini Kisii, Maangi aliwataka viongozi kuacha siasa na kufanya maendeleo kwa amani.
“Viongozi wote tulichaguliwa ili kuhakikisha wananchi wamepata maendeleo na wanaishi kwa umoja ili tuendeshe gurudumu la maendeleo pamoja, ili viongozi wanaofuata waweze kufuata mtindo ule ambao ni wa umoja," alisema Maangi.
Maangi aidha aliwahimiza viongonzi kutoingiza siasa kwa maendeleo, huku akisema wanapaswa kuhakikisha wanatimiza ahadi zote walizotoa.
“Naomba zile ahadi viongozi wenzangu mlizotoa muweze kuzitimiza ili tusonge mbele kama Jamii moja ya maendeleo,” aliongeza Maangi.
Aidha, Maangi aliomba watumishi wa Mungu kuendeleo kuombea nchi, hasa serikali kuu na ile ya kaunti ili kuwa na uongozi wa amani miongoni mwao .
“Ukifanya maendeleo utakuwa katika hali nzuri ya kuendelea kuongoza wananchi,” alisisitiza Maangi.