Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi amekanusha madai kuwa maeneo ya Jogoo na Daraja Moja yaliyoko katika mji wa Kisii, ni maeneo ambayo yanastahili kuwa katika Kaunti ya Nyamira.
Hii ni baada ya gazeti moja kuandika kuwa Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama alisema maeneo hayo yanafaa kuwa chini ya uongozi wa kaunti yake ya Nyamira.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi afisini mwake, Maangi alisema kuwa maeneo ya Jogoo na Daraja Moja yako katika Kaunti ya Kisii na kufutilia mbali madai ya Gavana Nyagarama.
Maangi aliwahakikishia wakazi wa eneo la Jogoo kuwa serikali ya Kaunti ya Kisii itaendelea kuwahudumia na kuwaletea maendeleo, na kuwaomba kutofuatilia mambo ambayo si ya ukweli.
“Wakazi wa Jogoo hawapaswi kuogopa chochote kwa vile wataendelea kuwa katika kaunti ya Kisii na serikali yetu itaendelea kuwahudumia kama kawaida,” alisema Maangi.
Yaana yanajiri huku serikali ya Kaunti ya Kisii na ile ya Nyamira zikiendelea kuzozana kuhusu mpaka wa Soko la Keroka.