Watu walio na uwezo wa kifedha(mabwenyenye) wametajwa kuwa wanaonyakua ardhi ya watu wanyonge katika maeneo mengi ya Nakuru.
Kulingana na aliyekuwa diwani wa zamani wa wadi ya Tinet David Sitienei, mabwenyenye hao hupata nafasi ya kunyakua ardhi za watu wanyonge kutokana na ukosefu wa hati miliki za ardhi katika ardhi nyingi.
Akizungumza Alhamisi katika eneo la Olenguruone, sitienei ameitaka serikali kushughulikiwa kwa mizozo ya mashamba ambayo inaendelea kuchipuka kila kuchao katika kaunti nzima ya Nakuru.
Alisema mizozo ya ardhi pia inatokana na hatua ya serikali kulifumbia macho swala hilo ambalo linaendelea kusababisha maafa katika maeneo mengi ya kaunti.
“Serikali ya kitaifa pamoja na za kaunti zinatakikana kuchukulia swala la ardhi kwa uzito la sivyo, huenda kaunti nyingi ambazo zinakumbwa na mizozo ya ardhi zikaingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe,” alisema Sitienei.