Share news tips with us here at Hivisasa

Machifu katika Kaunti ya Kisumu, wana kila sababu ya kutabasamu kufuatia mpango wa serikali kuu wa kuwanunulia pikipiki ili kurahisisha usafiri wao, kama hatua ya kuboresha huduma kwa wananchi.

Akizungumza katika hafla ya kupokeza pikipiki kumi kwa baadhi ya machifu siku ya Ijumaa, Kamishna wa Kaunti ya Kisumu John Elungata alisema kuwa mpango huo unanuia kuhakikisha kuwa machifu wote 50 katika Kaunti ya Kisumu, wanapokea pikipiki.

“Tumekuja hapa kwenye afisi zetu za kaunti ili kuwapa machifu pikipiki ambazo huenda zikaonekana kama zawadi ya mapema ya Krisimasi,” alisema Elungata.

Aliongeza, “Pikipiki hizi kubwa zenye nembo ya GK, zimenunuliwa na Wizara ya Masuala ya Ndani na Utawala ili kuwawezesha machifu kufanya kazi yao vyema.”

Olung’ata alisema kuwa machifu 40 waliosalia watapewa pikipiki hivi karibuni, katika awamu ya pili ya mpango huo.

Kamishna huyo alisema kuwa hutua hiyo inalenga kuwarahisishia machifu usafiri katika maeneo yao, hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kusafiri kuwahudumia wananchi kwa dharura.