Machifu wapatao kumi katika kaunti ya Uasin-Gishu ambao wameshindwa kukabiliana na pombe haramu ya chang’aa katika maeneo yao watafutwa kazi.
Kamishna wa kaunti hiyo Abdi Hassan amesema tayari machifu husika wamepokea barua zinazohusiana na mpango wa kuachishwa kazi.
Hassan alisema hatua hiyo ilichochewa na uzembe wa machifu hao ambao maeneo yao yangali yana pombe haramu hasa chang’aa.
Akihutubu katika mkutano na machifu mjini Eldoret leo hii katika hoteli ya Starbuck, Hassan alisema machifu husika wamekuwa wakionywa mara kwa mara lakini wamekataa kurekebisha.
Kulingana na Hassan, wengi wa machifu hao na manaibu wao wamekuwa wakipokea hongo kutoka kwa wagemaji na wauza pombe hiyo.
Hatua hiyo inalenga kuona kwamba agizo la rais Uhuru Kenyatta la kumaliza pombe haramu linaendelea kutekelezwa kote nchini.
“Tunajua ya kwamba kuna baadhi yenu ambao kazi yenu ni kupokea hongo kutoka kwa wagemaji wa pombe haramu ambapo imekuwa vigumu kumaliza pombe hiyo, hatuna msaada mwingine kwenyu ila ni kuachishwa kazi,” alisema Hassan.
Hassan aliwataka machifu hao kushirikiana na wadau wengine kama vile NACADA kufunga baa zote ambazo ziko katika makazi.
“Nimewapa juma moja kufunga baa zote ambazo ziko katika makazi, sheria hairuhusu baa kuwa karibu na makazi,” aliongezea.
Kiongozi huyo alitaka vilabu vyote vya usiku ambavyo viko nje ya katikati mwa mji wa Eloret kufungwa msimu huu wa likizo ya Krisimasi kama njia moja ya kulinda watoto dhidi ya kujiingiza katiika anasa.