Huenda hali ya usalama ikaimarika zaidi katika sehemu nyingi katika Kaunti ya Nyamira iwapo machifu watatumia pikipiki walizopokezwa kwa minajili ya kudumisha usalama vijijini.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiwahutubia wanahabari baada ya hafla ya kuwapokeza machifu pikipiki 44 siku ya Ijumaa, kamishna wa kaunti hiyo Josphine Onunga alisema anatumai machifu hawatakuwa na visingizio vya kutowahudumia wakazi wa maeneo yao maana pikipiki hizo zitawawezesha kusafiri kwa haraka.

"Sidhani kwamba machifu watakuwa tena na visingizio vya kutowahudumia wananchi kama siku za hapo awali walipokuwa wakilalamikia shida ya usafiri kwenye maeneo yao ya utawala. Pikipiki ambazo tumewapokeza hii leo zitawawezesha kusafiri kwa haraka," alisema Onunga.

Onunga aidha alisema machifu hao watapewa mafunzo ya kuendesha pikipiki hizo kabla yao ya kuanza kuzitumia.

"Kwa kuwa idadi kubwa ya machifu bado hawana mafunzo ya kuendesha pikipiki, nimewahimiza waende shuleni kujifunza jinsi ya kuendesha pikipiki hizo ndio wasije wakahusika kwenye ajali na mikosi inayoweza kuthibitiwa," aliongezea Onunga.