Machifu wote na manaibu wao katika kaunti ya Nyamira wameagizwa kuwachukulia hatua kali ya kisheria yeyote atakayehusika katika ukeketaji wa wasichana ili iwe funzo kwa wengine.
Agizo hilo limetolewa baada ya madai kuwa kuna baadhi ya wazazi katika kaunti hiyo wanaofanya shughuli hiyo kisiri na ni kinyume cha sheria na inatahadharisha afya ya wasichana.
Akizungumza siku ya Jumanne, kamishna wa kaunti ya Nyamira Josephine Onunga aliagiza machifu na manaibu wao kuwatia mbaroni na kuwafikisha mahakamani watakaohusika na shughuli ya kuwatahirisha wasichana.
Kulingana na kamishna huyo, Disemba ndio musimu ambao shughuli za ukeketaji huendelezwa kwa wingi jambo ambalo ni kinyume na sheria kwa watoto wasichana.
Hata hivyo, Onunga alisema ikiwa machifu hawatajitolea kupambana na visa hivyo, basi itakuwa vigumu kuikomesha shughuli hiyo ya kuwatahirisha wasichana, huku akiwahimiza kuwa katika mstari wa mbele kupambana na tohara ya wasichana.
“Kisheria, mtoto msichana haruhusiwi kutahiriwa na yeyeote atakiuka sheria hiyo atachukuliwa hatua kali ya kisheria,” alisema Josephine Onunga.
“Naomba kila chifu na manaibu wenu muwe katika mstari wa mbele kupambana na ukeketaji kwa watoto wasichana na yeyeote atakayehusika kwa shughuli hiyo atachukuliwa hatu kali ya kisheria,” aliongeza Onunga.