Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Waziri wa Usalama Joseph Nkaissery ametoa onyo kwa machifu ambao wanaruhusu pombe haramu kuendelea kuuzwa katika maeneo wanayosimamia.

Haya yamejiri huku serikali ikisema kuwa msako mkali dhidi ya pombe haramu utafanyika tena kote nchini, kufuatia ripoti kuibuka kuwa pombe hiyo imeanza kuuzwa tena.

Akizungumza siku ya Jumanne wakati wa mkutano wa amani katika eneo la Maella mjini Naivasha, Nkaissery alisema kuwa hata sita kumwachisha kazi chifu yeyote atakayezembea kazini, kama njia moja ya kupambana na pombe haramu.

"Machifu ndio maafisa wa serikali ambao wako karibu sana na wananchi, na wanastahili kujua kila biashara haramu inayofanywa katika kata yao. Kama eneo lako bado linauzwa pombe haramu, serikali haitasita kukufuta kazi. Tunataka watu ambao watatekeleza sheria zilizopo," alisema Nkaissery.

Uliokuwa mkoa wa kati wa Kenya unaongoza kwa kurejea kwa pombe hizo kulingana na Nkaissery.

Nkaissery alikuwa ameandamana na wabunge kadhaa ikiwemo Ferdinand Waititu wa Kabete na John Kihagi wa Naivasha.