Share news tips with us here at Hivisasa

Madalali wametajwa kuwa vyanzo vya mizozo ya ardhi inayoshuhudiwa katika maeneo mengi ya kaunti za Nakuru na Narok.

Wakizungumza na wanahabari siku ya Jumatano mjini Nakuru, wanachama wa kampuni ya kununua ardhi ya Natoli, walisema kuwa tangu madalali kuingilia kati uuzaji wa ardhi katika eneo la Ndabibi, mizozo ya ardhi imeshuhudiwa huku watu sita wakiwa wamepoteza maisha yao hadi kufikia sasa.

Kulingana na mkurugenzi wa shamba hilo, Jackson Ole Kateng’i, waliponunua shamba katika kampuni ya Agriculture Development Corporation, ADC, hawakuwa na matatizo yoyote lakini pindi madalali walipoingilia uuzaji wa ardhi, kumekuwa kukishuhudiwa katika eneo hilo.

Alitoa mfano na kizaazaa kilichoshuhudiwa majuzi katika chumba moja cha kuhifadhi maiti mjini Gilgil, ambapo mazishi yalisitishwa kutokana na mzozo wa ardhi, hatua aliyodai ilisababishwa na madalali walaghai wanaotumia ukora kuwauzia watu mashamba.

“Ikiwa madalali hawataondolewa katika uuzaji wa ardhi hapa Nakuru na hata kaunti zingine ambazo zimekuwa zikishuhudia mizozo ya ardhi nchini, basi tutaendelea kushuhudia maafa,” alisema Bw Ole Kateng’i.

Wanachama hao sasa wanataka wizara ya ardhi kuingilia kati na kusuuhisha mizozo ya ardhi katika eneo la Ndabibi kama ilivyofanya katika eneo la Maella.