Mzozo wa vituo vya kuhifadhi shehena katika bandari kuu jijini Mombasa unapoendelea kuchukua mkondo tofauti kila kukicha, madereva katika vituo husika wanahofu kuwa huenda wakapoteza kazi zao iwapo serikali haitalishughulikia suala hilo kwa haraka.
Madereva hao ambao wamekuwa wakikita kambi katika eneo la bandari wakisubiri kuona iwapo vituo vyao vya kazi vitafunguliwa, walisema kuwa maisha kwao yamekuwa changamoto tangu kufungwa kwa vituo vyao vya kufanyia kazi.
Wakiongozwa na Fareed Salimu siku ya Alhamisi, madereva hao walisema kuwa serikali inaonekana kufanya mambo kinyume na vile ilivyowaahidi Wakenya kuwa wataunda kazi ilhali wanendelea kuziuumbua.
“Tunahofia huenda wakubwa wetu wakatusimamisha kazi kama hali itaendelea hivi. Tunawaomba wahusika kutoka bandari pamoja na serikali yenyewe kufanya hima na kushughulikia suala hili mapema ili tuweze kuendelea na kazi zetu,” alisema Salimu.
Itakumbukwa kuwa mzozo wa vituo hivyo vya kuhifadhi shehena zinazopakiwa kutoka meli za kuingia bandarini ulianza mwishoni mwa mwaka jana.
Mzozo huo ulichacha mwanzo wa mwaka huu ambapo vituo kama Portside na AFS vilifungwa kwa muda hatua ambayo ilitajwa kuwa ya kisiasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vituo husika vilihusishwa na familia ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho.