Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josephine Onunga amewahimiza waendeshaji magari kuwa waangalifu hasa msimu huu wa likizo ndefu ya Desemba.
Akihutubia wananahabari afisini mwake siku ya Jumatatu, Onunga aliwahimiza wazazi kuwa waangalifu zaidi barabarani kwa kuwa watu wengi wanatarajiwa kusafiri kuenda likizo huku akiwahimiza kuzingatia sheria za barabarani.
"Yafaa kila mwendeshaji gari ahakikishe kuwa anazingatia sheria za barabarani anapowasafirisha watu hadi maeneo mbalimbali humu Nyamira. Hatua hiyo itahakikisha kuwa wananchi wanafika salama wanako taka kwenda ili kusherehekea krismasi na wenzao bila ya mikosi yeyote," alisema Onunga.
Onunga aidha aliwaonya waendeshaji magari dhidi yakuendesha magari wakiwa walevi akisema kuwa visa vingi vya ajali husababishwa na madereva walevi.
Alisisitiza kuwa madereva wa aina hiyo kamwe hawatavumiliwa.
"Kuna madereva wenye mazoea yakuendesha magari wakiwa walevi lakini wanapaswa kujua kuwa kamwe tabia hiyo haitoruhusiwa huku Nyamira. Maafisa wa usalama hawatasita kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa kuwa tunataka watu washerehekee krismasi bila ya matatizo yeyote," alisema Onunga.