Mwenyekiti wa chama cha madereva wa magari aina ya tuktuk mjini Nakuru sasa amefichua kuwa dereva wa gari aina ya tuktuk alikopatikana kahaba akiwa ameuwawa hakuwa mwanachama wa chama hicho.
John Njoroge kwenye mahojiano siku ya Jumanne alikariri kuwa iwapo dereva huyo angekuwa mwanachama wa chama hicho, basi hangeruhusiwa kuendesha biashara ile tena na isitoshe, angefurushwa kutoka chama hicho.
Njoroge alisema watafanya mkutano ili kuhakikisha kuwa visa kama hivyo havitokei tena kwenye magari yao.
Hata hivyo, aliwaomba wakaazi wa mji wa Nakuru wasiwe na hofu ya kutumia magari aina ya tuktuk huku akiwataka wamiliki wa magari hayo kufahamu kamili madereva wanaoendesha magari yao kabla ya kuwapa ajira.
Mikakati hii inafuatia kisa cha kahaba mmoja mjini Nakuru aliyepatikana ameuwawa ndani ya gari aina ya tuktuk katika mtaa wa Freehold viungani mwa mji wa Nakuru usiku wa kuamkia Jumamosi, wiki iliyopita.
Mwanamke huyo alipatikana na polisi waliokuwa wanashika doria katika mtaa huo wa freehold, akiwa na alama shingoni , hatua iliyoonyesha uwezekano wa kunyongwa.