Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wahudumu wa magari wameshauriwa kuwa waangalifu barabarani wanapoendesha biashara zao za uchukuzi ili kupunguza visa vya ajali barabarani la sivyo wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Hii ni baada ya gari kumgonga na kumua papo hapo mwanafunzi mmoja wa darasa la tano katika shule ya msingi ya Bosiango katika barabara ya kutoka Bosiango kuelekea Kebirigo siku ya Jumatatu.

Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Nyamira baada ya kisa hicho kufanyika Mkuu wa Polisi katika kaunti ya Nyamira Ricah Ongare aliwaonya madereva ambao hawazingatii sheria za barabarani na kusema yeyote atakayefumaniwa akivunja sheria hizo atakabiliwa kisheria.

“Naomba kila dereva kuwa mwangalifu barabarani maana ni wengi ambao wamepoteza maisha yao kwa kuhusika katika visa vya ajali barabarani kila wakati,” alisema Ongare

Kwa upande wa wakaazi nao  pia walitishia kuandamana kulalamikia barabara kutowekwa matuta jambo ambalo wamekuwa wakiomba serikali kuwawekea kwa muda mrefu sasa .

“Visa vya ajali vinafanyika katika barabara hii kila wakati kufuatia uendeshaji wa kasi maana hakuna matuta ambayo yanaweza kuwadibiti madereva, tutaandamana kulazimisha serikali kutuwekea matuta,” alisema Brightion Ombae, mkaazi.