Tangu Rais Uhuru Kenyatta kuzuru shirika la feri KFS, ziara iliyochangia usimamizi wa shirika hilo kubadilishwa miezi kadhaa iliyopita, mambo yanaonekana kubadilika huku wadau wa utalii wakiwa wa kwanza kutabasamu kutokana na mabadiliko hayo.
Hali ya usafiri sasa inatarajiwa kuwa nafuu kwa watalii wanaotumia kivuko hicho cha Likoni kuzuru maeneo mengine ya kusini mwa Pwani.
Hii ni baada ya shirika hilo kukubali ombi kutoka kwa wamiliki wa mahoteli kusini mwa Pwani ya kutaka magari ya utalii kuruhusiwa kupita katika kivuko hicho bila kupanga foleni.
Pendekezo hilo linakuja wakati ambapo sekta ya utalii imekuwa ikilalamika kwa madai kwamba watalii wamekuwa wakitumia muda mwingi kusafiri kutoka kisiwani Mombasa hadi maeneo ya kusini, kutokana na kucheleweshwa katika kivuko hicho.
Kaimu mkurugenzi wa Kenya Ferry Bakari Gowa alisema kuwa shirika hilo limekubali ombi hilo ili kunusuru sekta hiyo utalii.
“Tumeruhusu magari yote ya kubeba watalii yapite bila kupanga foleni ili wafike haraka wanakoenda,” alisema Gowa.
Watalii wanaovuka katika kivuko hicho mara nyingi huwa wanaelekea katika hoteli zinazopatikana katika maeneo ya Diani Ukunda miongoni mwa maeneo mengine katika Kaunti ya Kwale, ambapo serikali ya kaunti hiyo pia imeunga mkono hatua hiyo.
Hatua hiyo sasa inatarajia kuimarisha safari za watalii hao kwa kuhakikisha wanatumia muda mfupi zaidi ikilinganishwa na siku za hapo awali.
Kumekuwa na lalama kutoka kwa wamiliki wa mahoteli kusini mwa Pwani hapo awali kwamba biashara zao zinashuka kwani watalii huchukua muda mrefu katika kivuko hicho na pindi wanapofika hotelini, huwa wamechoka na kushindwa kufurahia ziara yao kama walivyokuwa wamepanga.
Gowa alichukua nafasi ya Mussa Hassan Musa aliyesimamishwa kazi mapema mwaka huu kutokana na madai ya usimamizi mbaya wa shirika hilo, jambo lililotajwa kuchangia pakubwa changamoto zilizokuwa zikishuhudiwa kivukoni humo.