Share news tips with us here at Hivisasa

Magavana wa kaunti za Kisii na Nyamira wamelaumiwa vikali kwa kutotimiza ahadi walizotoa za kuinua mji wa Keroka kimaendeleo.

Hii ni baada ya Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae na na mwenzake wa Nyamira John Nyagarama kukubaliana kuinua mji wa Keroka kwani mji huo uko mpakani wa kaunti hizo mbili.

Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo bunge la Kitutu Masaba, mbunge wa eneo hilo Timothy Bosire aliwalaumu magavana hao wawili kwa kukawia kuafikia na kutotimiza ahadi za maendeleo walizotoa kwa wakazi wa Keroka.

Kulingana na mbunge huyo, magavana hao wawili waliahidi kushirikiana pamoja kukarabati soko la keroka, barabara za mji huo, kuweka mataa ya usalama pamoja na kukusanya uchafu kila wakati mjini humo.

Bosire alisema hakuna chocchote kimeafikiwa tangu viongozi hao na wabunge wa kaunti hizo mbili kuwa na mkutano hapo awali, huku magavana hao wakiahidi kushirikiana kuinua mji wa Keroka kimaendeleo, jambo ambalo halijaafikiwa hadi sasa.

“Magana hawa wawili walitoa ahadi za kuinua mji wa Keroka, na kufikia sasa hakuna chochote kimefanywa, huo ni uongozi wa aina gani ?Naomba magavana hao kushirikiana na kutimiza ahadi zile walizotoa kwa wakazi pamoja na wafanyibiashara,” alisema Bosire.

Pia Bosire aliwataka magavana hao kueleza yale wamefanya katika mji huo tangu serikali za ugatuzi zianzishwe.

Mji wa Keroka uko mpakani wa Kaunti za Kisii na Nyamira, huku maendeleo yakifeli kufanywa kwa muda mrefu, jambo ambalo linawapelekea wafanyibiashara wa soko la hilo kuandamana kila wakati kulalamikia kutofanyiwa maendeleo kama soko zingine.