Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wafanyibiashara wa soko la Keroka wamewaomba gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama na mwenzake wa Kisii James Ongwae kujiunga pamoja na kuwaeleza bayana soko hilo liko katika kaunti ipi.

Wito huo umetolewa baada ya kusemekana kuwa soko hilo liko katika mpaka wa kaunti za Kisii na Kaunti ya Nyamira, jambo ambalo wafanyibishara wamesema limefanya wao kubaguliwa kimaendeleo kwa muda mrefu.

Kulingana na wafanyibiashara hao, hawana vyoo vya soko, hakuna ukarabati wa soko umewahi fanywa na kaunti hizo mbili, na kuna mazingira mabaya miongoni mwa mengine, huku wakishindwa ni kaunti ipi inastahili kuwasiadia ili kujiendeleza kiuchumi na kujiimarisha kibiashara.

Wakizungumza mnamo siku ya Jumanne katika soko hilo wakati wafanyibiashara hao waliandamana kulalamimkia kubaguliwa na serikali hizo mbili, wafanyibiashara hao wakiongozwa na Hesbon Onchiri na Christopher Mokua walisema wamepitia mengi maana hakuna serikali inataka kuwasaidia.

“Tunahitaji kuelezwa tuko katika kaunti ipi ili tufanyiwe maendeleo, na kuanzia leo hakuna ushuru itatozwa hapa Keroka,” alisema Mokua.

Wafanyibiashara hao walisema hutozwa ushuru kila siku, lakini hawajui pesa zao huenda wapi kwani hakuna maendeleo hufanywa katika soko hilo.

Wafanyibiashara hao walifunga afisi za watoza ushuru na kuwafurusha, huku wakiapa kutotozwa ushuru tena hadi wahakikishiwe usafi, wajengewe vyoo vya soko, wakarabatiwe soko na waelezwe soko hilo liko katika upande upi wa kaunti hizo mbili

Ushuru umekuwa ikikusanywa na serikali ya Kaunti ya Nyamira.