Mahakama ya Mombasa siku ya Alhamisi iliwapata na kesi ya kujibu washukiwa wawili wanaodai kuhusika na shambulizi la kigaidi lililotekelezwa katika eneo la Mpeketoni, Kaunti ya Lamu mwaka wa 2014.
Akitoa uamuzi huo, hakimu Martin Muya alisema kuwa upande wa mashtaka umetoa ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa mfanyibiashara Mahadi Swaleh Mahadi na Dyana Suleiman wanafaa kufunguliwa mashtaka.
Wawili hao walitiwa nguvuni na idara ya usalama kwa madai ya kuhusika katika shambulizi la Mpeketoni mwezi Juni, 2014, shambulizi ambalo lilisababisha vifo vya watu zaidi 60.
Hakimu Muya sasa ameuagiza upande wa mashtaka kuendelea na kesi hiyo.
Hata hivyo, washukiwa hao kupitia wakili wao wamekana kuhusika na shambulizi hilo na kushikilia kuwa hawana hatia na kuwa wako tayari kujitetea.