Mahakama kuu ya Nakuru sasa imedinda kutoa agizo la kumruhusu mshukiwa wa mauwaji kukaa nje kwa dhamana akisubiri hukumu kutolewa dhidi yake.
Ni uamuzi ambao ulitolewa na jaji wa mahakama kuu Mary Odero siku ya Ijumaa katika kesi hiyo ya Stephen Karanja anayedaiwa kumuuwa babake wa kambo Paul Mugo kwa kumgonga kwa rungu kichwani mnamo tarehe 15 Machi mwaka wa 2011 katika kijiji cha Nyakiambi, kaunti ya Laikipia.
Akitoa uamuzi huo, jaji huyo alikariri kwamba uamuzi wake ulitokana na kuwa mshtakiwa alikuwa amedaiwa kutishia kumuua mwanawe dadake na hivyo usalama wa familia yake ulihofiwa.
Aidha, mwendesha mashtaka wa serikali afahamisha mahakama ya kwamba familia ya mshtakiwa ilikuwa tayari imemkana na hivyo hakuwa na mahala pa kwenda iwapo angewachiliwa.
Aliongeza kuwa mshukiwa huyo hana ajira na hivyo kulikuwa na uwezekano wake kutoweka kwani shtaka lake lina uwezekano wa kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Hukumu dhidi ya mshtakiwa huyo sasa inatarajiwa kutolewa tarehe 4 mwezi February mwaka huu .