Uamuzi wa kesi inayowakabili maafisa wawili wa polisi wanaodaiwa kumuuwa Kwekwe Mwandaza umeahirishwa hadi Februari 10, 2016.
Hii ni baada ya Jaji Martin Muya kuhairisha kesi hiyo siku ya Ijumaa kwa kusema kuwa ushahidi hauko tayari.
Washtakiwa katika kesi hii ni maafisa wa polisi Veronica Gitahi na Issa Mzee.
Stakabadhi zilizowasilishwa zimebaini kuwa wakili wa washtakiwa, Jared Magolo, amekubali kwamba marehemu Kwekwe Mwandaza aliuawa kwa kupigwa risasi, lakini bado wanachunguza kilichosababisha tukio hilo.
Naye wakili wa serikali Peter Kiprop, alisema kulingana na ushahidi uliotolewa ikiwemo ripoti ya daktari, marehemu alifariki kutokana na majeraha ya risasi.
Shahidi wa mwisho kutoa ushahidi katika mahakama kuu mjini Mombasa alikuwa ni Job Ouma, afisa wa ujasusi kutoka Kinango.
Ouma aliambia mahakama kuwa polisi wangali wanawasaka watu wanne waliohusishwa na uhalifu na ambao walikuwa wakisakwa kabla ya Kwekwe Mwandaza kuuawa, akiwemo mjombake George Zani.
Mnamo April 23 ,2015, wadogo wa Kwekwe waliambia mahakama kuwa walilazimishwa kupiga magoti juu ya damu ya dada yao baada ya kupigwa.
Afisa wa polisi Mwinyi Bakari aliambia mahakama kuu mnamo Julai 24, 2015, kwamba alimuona afisa wa upelelezi Veronica Gitai pamoja na Issa Mzee wakibeba mwili wa mwendazake Kwekwe Mwandaza akiwa hali maututi baada ya kumpiga risasi huko Maweu, Kaunti ya Kwale.
Afisa wa upelelezi Veronicah Gitahi pamoja na Chief Constable Issa Mzee walipatikana na kesi ya kujibu katika mauaji ya Kwekwe Mwandaza, msichana aliyekuwa na umri wa miaka 14 huko Kinango kaunti ya Kwale mnamo 2014.