Idara ya mahakama sasa imetakiwa kujibidiisha kukamilisha kwa haraka kesi za watoto walio kwenye rumande.
Wito huo umetolewa na meneja wa kituo cha urekebishaji wa tabia cha Nakuru Remand Childrens' Home kilicho kwenye mtaa wa Bondeni viungani mwa mji wa Nakuru Lorna Sang.
Kwenye mahojiano na mwandhisi huyu katika kituo hicho Alhamisi, Sang alisema amelalamikia jinsi kesi zinazowakabili watoto walio kwenye vituo hivyo zinaendeshwa kwa upole.
Anasema kwamba kulingana na sheria, watoto walio kwenye vituo hivyo vye kurekebisha mienendo wanafaa kukaa kwenye vituo hivyo kwa muda wa miezi mitatu pekee, lakini hata hivyo, kutokana na kesi kuchukua muda mrefu kortini, watoto hawa husalia kwenye vituo hivyo kwa zaidi ya miezi mitatu.
Ni hatua anayosema inawapelekea kupoteza muda mwingi sana huku wenzao wakiendelea na maisha.
"Sheria ya watoto inaonyesha kwamba wanafaa kukaa kwenye vituo hivi kwa muda wa miezi mitatu. Hata hivyo, watoto wengine wamekaa hapa kwa muda zaidi. Kutokana na hilo, tunaomba mahakama iweze kuharakisha kesi za watoto," alisema Sang.
"Iwapo ni mtoto ameshtakiwa au ikiwa ni yeye anayefaa kutoa ushahidi, kesi yake inafaa kuharakishwa kwa kuwa mtoto akiwa hapa, hawezi kusoma au kuendelea maishani," aliongeza Sang.
Ingawa amekiri kwamba watoto hao huwa hawapokei masomo ya darasani wakiwa kenye rumande, huwa wanajibidiisha kuhakikisha kwamba wanajifunza mambo mbalimbali .
"Huwa tunahakikisha kwamba tunawafunza maswala mbalibali kama vile kuhusiana na haki zao kama watoto, taaluma wanazoweza kutumia maishani na isitoshe, huwa wanahusika kwenye michezo mbalimbali. Huwa tuwawahusisha kwenye shughuli mbalimbali ili wasiwe na muda wa kupoteza kwani huenda wakawa wenye mawazo mengi iwapo hilo litattendeka," aliongeza.