Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idara ya Mahakama nchini imeshinikizwa kuidhinisha mikakati mwafaka ya kuwaadhibu viongozi wa kisiasa, maafisa wa idara za umma na wakazi kwa jumla watakaopatikana wakieneza ujumbe wa chuki na uchochezi.

Kulingana na mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, iwapo idara ya mahakama nchini itaibuka na adhabu kali dhidi ya watu kama hao, basi taifa hili litakuwa la amani na umoja.

Nassir alisema hatua hiyo itawalazimu viongozi kubadili mwenendo na kueneza ujumbe wa amani miongoni mwa wakenya.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Nassir alisema kwamba hatua ya baadhi ya viongozi kutoa matamshi ya chuki na uchochezi katika mikutano ya hadhara bila kuchukuliwa hatua za kisheria ina shusha hadhi ya taifa na huenda ikazua mafarakano.

Mbunge huyo wa Mvita alipendekeza idara ya mahakama kuwafungulia mashtaka na kuwahukumu watakaopatikana wakitoa matamshi ya chuki na uchochezi kama njia mojawapo ya kusitisha malumbano ya hadharani.

"Tungependa kuona idara ya mahakama inaweka mikakati dhabiti ya kuadhibu kisawasawa viongozi waonatoa matamshi ya chuki ili kuzuia kuwagonganisha Wakenya na kuzua mafarakano,” alisema Nassir.

Kauli ya kiongozi huyo imejiri baada ya kushuhudiwa visa vya viongozi mbalimbali wa kisiasa wakitoa matamshi ya chuki na uchochezi hahdarani.