Share news tips with us here at Hivisasa

Mahakama kuu ya Nakuru imewataka viongozi kutoka afisi za jimbo la Nakuru na bunge lake kujibu kwa kipindi cha wiki mbili zijazo mashtaka kuhusu kumwondoa afisini spika wa bunge la jimbo la Nakuru Susan Kihika.

Jaji Maureen Odero ameitaka serikali ya kaunti, bodi ya bunge la kaunti pamoja na karani wa bunge hilo kujibu mashtaka hayo kwa kipindi hicho, kabla ya kesi husika kusikizwa mnamo machi 22.

Katika kesi hiyo aidha MCA mteule Margaret Wanjiru Kiiru amemshtaki karani wa bunge kwa kukosa kuwasilisha mswada wa kumwondoa spika wa bunge hilo Susan Kihika.

Bi wanjiru ameeleza mahaka hiyo kuwa karani Joseph Malinda alikosa kuwasilisha mswada huo na hivyo mswada huo kukosa kutajwa katika bunge ili ujadiliwe.

Kwa sasa ameitaka mahakama kutafsiri na kuweka bayana sheria zinazobaini masuala ya kumwondoa ama kutokuwa na imani na mtu aliye afisini ili kuwezesha mswada huo kupita, akihoji tayari ana sahihi za kutosha za kumwondoa spika huyo huku akimshtumu karani huyo kwa kukosa kutekeleza wajibu na mamlaka yake ipasavyo.

Spika Susan Kihika anashtakiwa kwa utumizi mbaya wa afisi, usimamizi mbaya sawia na utumizi mbaya wa hela za bunge mbali na ufisadi, yote yakidaiwa kuwa msingi tosha kwa spika huyo kung’olewa afisini.

Hata hivyo Malinda amedai kuwa Bi Wanjiru alimtumia barua mnamo machi 18, 2015 ambapo alidai kuondoa mswada huo hadi siku nyingine na kuwa sababu tosha kuwa yeye kama karani hangeuwasilisha mswada huo bungeni ili kujadiliwa.