Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, wameeleza furaha yao kuhusiana na ziara ya kiongozi wa Kanisa la Kikatoliki Papa Francis anayetarajiwa humu nchini mwezi huu.

Viongozi hao walisema kuwa ziara hiyo inakuja wakati mwafaka kwa Wakenya ikizingatiwa kuwa viongozi wamekua wakitoa matamshi ya uchochezi.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, katibu mtendaji wa baraza hilo, Sheikh Mohammed Khalifa, alimtaka kiongozi huyo wa Kanisa la Katoliki kuwasihi wanasiasa kutotoa matamshi ya uchochezi katika ziara yake ya humu nchini.

“Namwomba Papa Francis kuwasihi wanasiasa kutotoa matamshi ya uchochezi nchini na badala yake kuzingatia maendeleo ya taifa,” alisema Sheikh Khalifa.

Aidha, Khalifa alisema ziara hiyo inaonyesha umoja wa dini zote nchini na kutupilia mbali mgawanyiko kwa misingi ya dini.

Wakati huo huo, amemtaka Papa Francis kuzungumzia suala la wanafunzi wa Kiislamu kutopewa uhuru wao wa kimavazi katika shule zinazodhaminiwa na Wakristo.