Share news tips with us here at Hivisasa

Biwi la simanzi limetanda katika sehemu ya Nyaikuro, wilayani Manga, Kaunti ya Nyamira baada ya mwili wa mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 70 kupatikana ndani ya nyumba yake siku ya Jumatano.

Akithibitisha kisa hicho, chifu wa kata ya Kitutu Mashariki Jane Matara alisema kuwa mwili wa marehemu, Esther Bwoma, ambaye amekuwa akiishi na mfanyikazi wake ulipatikana sebuleni huku ukiwa na damu na watu waliokuwa wameenda kuchukua maziwa kutoka kwake.

"Watu ambao huchukua maziwa kila siku kutoka kwa boma ya marehemu walifika na kumkosa mfanyikazi wake na walipogonga mlango, hawakupata jibu. Walifungua mlangu ambao haukuwa umefungwa na kupata mwili wa Bwoma ukiwa sebuleni,” alisema Matara.

Bi Matara alisema kuwa mfanyikazi wake marehemu kutoka eneo la magharibi mwa Kenya hajulikani aliko na maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi kubaini ukweli wa mambo.

"Cha kushangaza ni kwamba mfanyikazi wake hajulikani aliko, lakini maafisa wa polisi wamefika na wameanza uchunguzi,” alisema Matara.