Hali ya sintofahamu inazingira idara ya polisi mjini Naivasha baada ya askari mmoja wa kulinda magereza eneo hilo kupoteza kupoteza kwa bunduki yake.
Askari huyo anayehudumu katika gereza ndogo la Naivasha, alivamiwa na majambazi Alhamisi alipokuwa akilinda karakana moja inayomilikiwa na idara ya magereza karibu na barabara kuu ya Nairobi kuelekea Nakuru.
Pindi tu baada ya kuiba bunduki hiyo aina ya G3 majambazi hao walivamia duka moja la Jumla mjini humo na kuiba kiasi cha pesa ambacho hakijulikani pamoja na na mali nyingine kutoka kwa mmiliki wa duka hilo. Aidha wateja waliokuwepo hawakusazwa kwani pia waliporwa.
Hata hivyo baadhi ya wakaazi wa Naivasha walilalamikia utepetevu wa polisi kwani duka kwa jina ‘Super Duka’ limo umbali usiozidi mita 150 kutoka kwenye makaazi ya polisi mjini humo. Walieezea hofu kwamba kama silaha hiyo haitapatikana, huenda ikatumiwa kuwahangaisha.
“Huenda hata wanaotuhangaisha ni maafisa wa polisi wanaojifanya wezi, ama wanaoshirikiana na wezi,” Monicah Wambui alisema.
OCPD wa Naivasha Titus Munyoki amedhibitisha tukio hilo akisema kuwa wameanzisha uchunguzi kutafuta bunduki hiyo.