Hali ya wasi wasi ilitanda Jumatatu usiku mjini Naivasha baada ya genge la majambazi kuvamia duka moja lenye umaarufu mkubwa na kuiba pesa na mali nyingine ya dhamana.
Wezi hao ambao idadi yao haijajulikana walivamia duka la Kanini Haraka na kuiba shilingi milioni 1.2 na bidhaa zingine.
Hata hivyo walinzi wawili wa kibinafsi waliokuwa wakilinda duka hilo hawakupatikana pindi tu baada ya wizi huo.
Mkazi mmoja kwa jina Jacob Mbugua amesema kuwa wezi hao walivamia usiku wa manane, kabla ya kuvunja na kupora duka hilo.
“Wezi hao walivunja mlango mmoja na kuelekea hadi katika afisi ya fedha na ndipo waliweza kupata pesa hizo,” alisema Mbugua.
Kulingana naye, dhamana ya bei ya bidhaa zingine zilizoibiwa haikujulikana mara moja huku wafanyikazi wa duka hilo wakijawa na hofu.
Afisaa mmoja wa polisi, na ambaye hakutaka kutajwa jina, amedhibitisha tukio hilo na kusema kuwa walikuwa wakiwatafuta walinzi hao ili waweze kulezea ni nini kilichotendeka.
“Huenda wizi huu ulikuwa umepangwa kwa kindani kwa sababu ni wafanyikazi wachache wanaoweza kuingia katika afisi ya fedha katika duka hili,” alisema afisa huyo.