Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa upelelezi wa tume ya kupambana na ufisadi nchini wamekuwa wakikagua stakabadhi zilizotwaliwa kutoka kwa nyumba na maofisi ya maafisa wawili wakuu wa Kaunti ya Nakuru.

Naibu mwelekezi wa tume hiyo kanda ya kusini mwa Bonde la Ufa Gilbert Lukhoba amesema kuwa maafisa hao wanafanya uchunguzi ya madai ya ubadhirifu wa fedha dhidi ya maafisa hao wawili.

"Pindi tutakapomaliza uchunguzi wetu, tutatoa ripoti kuhusiana na uchunguzi wetu," aliongeza Lukhoba.

Stakabadhi hizo ni pamoja na vyeti vya umiliki wa mashamba yanayomilikiwa na maafisa hao, maelezo kutoka kwa benki, stakabadhi zingine za umliki wa mali ya maafisa hao na rekodi za matumizi ya fedha.

Wiki iliyopita makachero wa tume hiyo walivamia nyumbani kwa maafisa hao pamoja na afisi za mkurugenzi mkuu wa mipango na fedha wa kaunti Anne Nyambura Njenga, na afisa mwingine wa idara hiyo Billy Kiprotich, huku vita vya kupigana na ufisadi vikishika kasi katika kaunti hiyo ya Nakuru.