Shirika la kutetea haki za kibinadamu Muhuri mjini Mombasa limesema kuwa watoto wanaozurura mitaani wako katika hatari kubwa ya kujiunga na makundi haramu kutokana na hali duni ya maisha.
Wakiongea katika uwanja wa Makadara mjini humo siku ya Jumanne, maafisa wa shirika hilo waliangazia ripoti yaumoja wa kimataifa inayoonyesha kuwa ukosefu wa ajira pia umechangia katika tatizo hilo.
Akiongea wakati wa kongamano hilo, Bi Topista Juma ambaye ni afisa kutoka shirika hilo kitengo cha watoto aliongeza kuwa utafiti wao unaonyesha kuwa baadhi yao hutumiwa kuuza mihadarati.
“Watoto wanapitia changamoto nyingi, tumekutana na watoto kadhaa wa mitaani na wakatueleza matatizo yao. Wanatamani kuishi kama watoto wengine lakini umaskini unawafanya wanatumiwa kuuza mihadarati,” alisema Bi Juma.
Miezi kadhaa iliyopita kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa alitoa onyo kuwa idara ya polisi ilikuwa imepata taarifa kuwa makundi ya kigaidi yanalenga kuwahusisha watoto wa mitaani katika shughuli zao.