Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi amesema kuwa wazazi mjini Mombasa wanachangia pakubwa katika visa vya watoto wadogo kujihusisha na makundi ya wahalifu.
Mwinyi alisema kuwa wazazi wengi mjini Mombasa hawafuatilii mienendo ya watoto wao huku akitaja swala hilo kama tishio kubwa katika maisha ya baadae eneo hilo.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Mwinyi alisema kuwa serikali haiwezi kutatua changamoto ya makundi ya wahalifu iwapo wazazi hawatachukua hatua ya kwanza.
“Watoto wanatumia muda mrefu nje kuliko wanapokuwa nyumbani na wanakutana na watu wengi kule nje wanaowafunza mambo mengi maovu. Kila mzazi anafaa kuchukua jukumu lake,” alisema Omar.
Mbunge huyo ametaja vijana wa eneo la Pwani kama wenye uwezo wa kujiendeleza na kufanya mambo makubwa katika jamii.
Hata hivyo, alisema kuwa kadri wazazi wanavyopuuza swala hilo, ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya.
Aidha, aliongeza kuwa jambo la kuzingatia miongoni mwa vijana Mombasa ni elimu, kwani hiyo ndio itakayobadilisha taswira ya eneo hilo.
“Kama mbunge, nitashirikiana na washikadau wote katika elimu ili tubadilishe ile dhana kwamba shule zetu ni za kwenda tu na kurudi, bali ziwe za kutoa watu wenye manufaa,” alisema Mwinyi.
Matamshi ya mbunge huyo kuhusu maadili ya watoto yanakuja huku idara ya polisi ikiendeleza msako mkali dhidi ya makundi ya wahalifu yanayowaangaisha wakaazi katika eneo hilo.
Makundi ya Wakali Kwanza na Wakali Wao yametajwa kuwa hatari zaidi eneo la Kisauni huku ikisemekana kwamba wengi wao ni watoto wadogo waliotoroka shuleni.