Kamanda mkuu wa Polisi Kaunti ya Mombasa Francis Wanjohi amesema kwamba makundi ya kihalifu ya 'Wakali Kwanza' na 'Wakali Wao' yanayowahangisha wakazi wa eneo la Kisauni mjini Mombasa lazima yatakabiliwa.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Wanjohi alisema kwamba maafisa wa polisi wako nyanjani kuyasaka makundi hayo ya kihalifu ili kuwatia nguvuni na kuimarisha usalama wa eneo hilo.
Wanjohi amewahakikisha wakazi wa kaunti ya Mombasa hasa eneo la Kisauni, Mtopanga, Bamburi na Mishomoro kuwa makundi hayo yatakabiliwa kikamilifu na kuonyeshwa kwa wakazi majambazi sugu wanaowahangisha wakazi kila uchao.
“Tunawahakikishia wakazi wa Mombasa kuwa maafisa wa polisi wanayasaka makundu hayo ya kihalifu na lazima yatakabiliwa kikamilifu ili kuimarisha usalama wa eneo la Kisauni na kaunti nzima ya Mombasa,” alisema Wanjohi.
Hatua ya Kamanda huyo mkuu wa polisi amesema kwamba oparesheni ya kuwasaka wahalifu hao itazidishwa ili kuona kwamba usalama wa kaunti nzima ya Mombasa inaimarishwa.