Mwanamke mmoja wa umri wa miaka thelathini amekamatwa na maafisa wa polisi baada ya kumpiga mwanawe na kumkata kata mwilini kwa kutumia kisu eneo la Thogoto.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamke huyo anadaiwa kuanza kumwadhibu mtoto huyo wa miaka sita baada ya kumtuma dukani kisha mtoto huyo akapoteza pesa alipokuwa akienda dukani. 

Majirani wa mshukiwa wanamtaja mwanamke huyo kuwa mama wa kambo wa mtoto huyo baada ya mamake mzazi kufariki miaka miwili iliyopita. 

Hannington Maina, jirani mmoja, akizungumza baada ya tukio hilo alisema kuwa mtoto huyo huadhibiwa vibaya kila siku, na juhudi zao kumuonya mama huyo hazikufua dafu.

Akidhibitisha kisa hicho, Mkuu wa polisi wa Kikuyu Mutune Maweu alisema visa hivi vimeongezeka miongoni mwa wazazi na ni hatia kubwa.

Aidha alisema kuwa kuadhibu mtoto haikumaanisha kumpiga na silaha au kutumia kisu. 

Afisa huyo aliongeza kuwa mtoto huyo alikuwa amekatwa katwa mkono, mguu na hata usoni kwa kisu na mama huyo.

"Ningependa kuwaonya wazazi ambao hukiuka msingi wa kuadhibu mtoto na kutenda uhalifu kuwa sheria itachukuwa mkondo wake," alisema Maweu.

Alidhibitisha kuwa mtoto huyo alikuwa katika hali isiyo ya hatari, huku akisema kuwa alikuwa anapokea matibabu katika hospitali ya Kikuyu.