Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa eneo bunge la Bobasi Steve Manoti amewaonya wasimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika bunge lake pamoja na wa bodi za shule dhidi ya utumizi mbaya wa pesa za hazina za ustawi maeneo bunge kuwa atawachukulia hatua kali za kisheria.

Akizungumza katika eneo bunge lake siku ya Jumanne, Manoti alisema wasimamizi wa miradi ya maendeleo na wale wa kila shule sharti waeleze bayana jinsi pesa anazowakabidhi zinatumika ili kuonyesha uwazi.

Aidha, aliwaonya wale ambao watashindwa kueleza jinsi wametumia pesa hizo kuwa watakabiliwa na sheria kali, huku akiongeza kuwa pesa hizo ni za watozwa ushuru na kuna haja ya kila mwananchi kuona jinsi zinafanya kazi.

Mbunge huyo aliapa kuwa atajaribu kila awezalo kuhakikisha kuwa pesa za watozwa ushuru zinafanya maendeleo kikamilifu kwa njia ya pekee na uwazi.

“Yeyote atakayepatika akitumia pesa vibaya ambazo ni za maendeleo atakabiliwa kisheria. Nawaonya wale wako na hiyo tabia ya kuvuja pesa za wananchi, nikiwa mbunge hilo sitaliruhusu kamwe,” alisema Manoti.