Huenda ujio wa Rais Uhuru Kenyatta eneo la Pwani mapema wiki hii ukabadili mkondo wa siasa za eneo hilo.
Ikumbukwe kuwa eneo la Pwani ni ngome ya mrengo pinzani wa Cord, lakini kuna kila dalili za kuonyesha kuwa mrengo uliomadarakani unajipanga kuteka kura za wakaazi wa ukanda huo.
Kuteuliwa kwa Mbunge wa Malindi Dan Kazungu kama Waziri wa Madini ni moja wapo ya ishara kamili kuwa serikali ina mpango wa kujaribu kupima umaarufu wake katika eneo la Pwani, kwani kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Malindi mnamo Machi 7, 2016 kutabaini mbivu na mbichi.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa Cord wameamua kuiunga mkono serikali, wakiongozwa na Mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani, Mbunge wa Kilifi Kazkazini Gideon Mungaro na Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Kwale Zainab Chidzuga, waliotangaza hadharani azma yao ya kufanya kazi na serikali.
Viongozi wengine waliotishia kuvihama vyama vyao ni pamoja na Mbunge wa Ganze Peter Shehe, Mbunge wa Kilifi Kusini Mustapha Iddi, Mbunge wa Rabai James Kamote na Mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga.
Suleiman Shahbal, ambaye ni mpinzani mkuu wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho pamoja na mwanasiasa mkongwe ambaye pia alikuwa Mbunge wa zamani wa Changamwe Ramadhan Kajembe, walisalimu amri na hawakusazwa katika mchakato wa kuvihama vyama vyao na kujiunga na Jubilee.
Shahbal alikihama chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka, huku Kajembe akihama ODM.
Mbunge wa Nyali, Hezron Awiti, naye ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha ugavana Kaunti ya Mombasa kwa tikiti ya ODM. Hatua ambayo inakadiriwa kugawanya wapiga kura wa kaunti.
Hapo awali, masaibu ya Cord yalidhihirika pale Mbunge wa Kinango Gonzi Rai alipohama chama cha Ford Kenya kilichochini ya mrengo huo na kujiunga na chama cha TNA dakika za mwisho kabla ya uchaguzi.
Rai, ambaye ni rafiki wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta alikinyakuwa kiti cha ubunge katika eneo bunge la Kinango, na ikawa ni dhihirisho kamili kuwa Cord inapoteza umaarufu.
Duru za kuaminika zinaarifu kuwa Balozi wa Tanzania, Chirau Ali Mwakwere atapigania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Kwale kupitia chama cha Jubilee, hatua ambayo itawagawanya wakaazi wa eneo hilo ambalo linaongozwa na Gavana Salim Mvurya.
Siasa za ukanda wa Pwani zinageuza mkondo, na iwapo mrengo wa Cord hautakuwa makini na kucheza kadi zake vilivyo, basi serikali haitakuwa na wakati mgumu kuwashawishi wakaazi wa Pwani kuiunga mkono.
Dalili zote zinaonyesha kuwa baadhi ya viongozi watahama vyama vyao na kutumikia chama kilichobuniwa hivi majuzi cha Jubilee Party ifikapo uchaguzi mkuu mwaka wa 2017.