Share news tips with us here at Hivisasa

Takriban asilimia 68% ya wananchi watukufu wa Kenya, walikuwa na matumaini makuu na kupitisha katiba ya majimbo Agosti 2010.

Katiba hiyo ilikuwa ikipigiwa debe na viongozi tofauti nchini kwa minajili ya kuleta maendeleo mashinani, huku kinaya kikuu kikidhihirika mapema mno kwa malumbano ya viongozi na kuonyeshana ubabe wa kisiasa kila kukicha.

Serikali za ugatuzi ambazo zina mamlaka zaidi kuongoza kaunti tofauti nchini, zinaonekana kulemaza juhudi na malengo mahsusi ya maendeleo yaliyoelezwa katika katiba mpya, ikiwemo miundo msingi, ustawishaji wa uchumi katika kaunti, kushukisha gharama ya maisha kwa mwananchi mchochole, uwepo wa amani na usalama kwa mwananchi miongoni mwa mengine mengi.

Aidha, kinaya kikuu bado kinaonekana kukithiri kufuatia kupuuziliwa mbali kwa mambo msingi yanayoathiri jamii, ikiwemo ufisadi miongoni mwa viongozi katika kaunti, ukosefu wa usalama kwa baadhi ya maeneo, ongezeko la uhaba wa ajira huku gharama ya maisha ikipanda maradufu kila kukicha.

Maendeleo ya viongozi yanaonekana tu majukwaani wanapozozana huku wakinyosheana vidole vya lawama, nakusahau kabisa kauli mbiu ya katiba mpya na ni kwanini wameteuliwa wawe viongozi.

Pia kumekuwa na mtindo wa viongozi kuasi sheria ya vyama vyao vilivyo wapeleka bungeni na kuhama kuelekea mirengo mingine kwa maslahi yao binafsi.

Je, ubabe wa kisiasa ndio kauli mbiu inayopelekea viongozi wengine kuhama vyama vyao au ni tamaa tu za viongozi binafsi?

Utakubaliana nami kuwa kila kitu kwa sasa kinaendeshwa katika mienendo ya kisiasa, suala linalopelekea baadhi ya wananchi waliopinga sera za viongozi fulani kukosa msaada wowote baada ya wao kuibuka washindi.

Maendeleo kwa baadhi ya maeneo nchini yanalemazwa na viongozi hao wanaopenda kushusha hadhi za jamii fulani. Swali ni je nani hakosei na nani aliye sawa ulimwenguni?

Je, mwamko upi unaendele katika siasa za ubabe nchini?