Uhamasisho kuhusu jinsi ya kuimarisha amani hasa wakati wa uchaguzi mkuu zitaendelezwa na serikali ya Marekani hapa nchini.
Balozi wa Marekani Humu nchini Robert Godec amesema kuwa hamasa hiyo itahakikisha kuwa wakenya hawachochewi na wanasiasa katika kuzua fujo.
Akiwahutubia wanahabari siku ya Jumatano, mjini Mombasa, Godec aliongeza kuwa amani na usalama ni maswala ambayo lazima yatiliwe manani na viongozi wote.
Balozi huyo aliongeza kuwa ili kuepuka ghasia, lazima wanasiasa kukoma kutoa matamshi ya uchochezi nchini, na akawasihi wakenya kutofuata mienendo ya wanasiasa wasiokuwa na msingi wa umoja na kuboresha amani.
Godec aliwataka wakenya kuepuka vurugo kama lililotokea mwaka 2007, ambapo watu wengi waliuawa na wengine kuachwa bila makao.
Naye Gavana wa kaunti ya Kilifi Amason Kingi amewataka wanasiasa wote kuhakikisha kuwa wametafuta njia mwafaka ya kutafuta kura badala ya kuwagawanya wananchi wa eneo la Pwani.