Idara ya Usalama katika Kaunti ya Mombasa imebaini kuwepo kwa wafausi wa kundi la kigaidi la al-Shabaab mjini Mombasa wanaowasajili vijana wanao randaranda mtaani kujiunga na kundi hilo nchini Somali.
Kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa, tayari idara ya upelelezi imekusanya ripoti ya majina ya wafuasi hao na uchunguzi umeanzishwa.
Marwa alisema kuwa jamaa hao wako katika maeneo ya Majengo, Kisauni na Mji wa Kale.
Kwenye mkao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Marwa alisema kwamba wafuasi wa kundi hilo la kigaidi wanawasajili vijana chini ya umri wa miaka 15 na kuwaahidi kuwapa mishahara mikubwa huku akisema kwamba serikali kamwe haitalegeza kamba kuyakabili makundi hayo.
Marwa amewataka maafisa wa usalama kuwatia nguvuni vijana hao pamoja na genge hilo huku akiwaonya vijana kujitenga na watu kama hao wenye nia ya kuwatumia vibaya, kwani serikali itawakabili barabara ili kuimarisha usalama wa wananchi.
"Lazima hawa jamaa watiwe nguvuni kabla ya kufanya mashambulizi kwani wanahatarisha maisha ya wakazi. Tayari tumepata majina yao na tunawachunguza. Lazima watakabiliwa kwani serikali iko macho,” alisema Kamishna Marwa.
Hata hivyo Kamishna huyo wa kaunti ya Mombasa amewahakikisha wakazi usalama dhabiti huku akiwataka kushirikiana na maafisa wa usalama katika kuwapa habari muhimu kuhusu washukiwa wa ugaidi na wahalifu ili watiwe nguvuni.