Mshukiwa mmoja ambaye anaaminika kuwa kiongozi wa mojawapo ya magenge ya vijana ambao wanatekeleza uovu katika jiji la Mombasa ametiwa mbaroni na idara ya polisi kwenye kaunti hiyo.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari siku ya Jumatano jijini Mombasa, kamishna wa Kaunti hiyo Nelson Marwa alisema kuwa mshukiwa yuko chini ya mikono ya maafisa wa polisi, na anadhaniwa kuwa miongoni mwa viongozi wa makundi ya vijana ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakazi katika mitaa mbali mbali ya Kaunti hiyo.
Marwa alisema kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na uhalifu, na maafisa wa polisi wataendelea kumzuilia mshukiwa huku wakimfanyia uchunguzi ili kupata habari zaidi kuhusu wahalifu wenzake na kutaka kujua alivyopata silaha alizokuwa nazo.
“Mshukiwa huyu anaamika kuwa kiongozi wa genge moja la vijana wanaotekeleza uhalifu hapa jijini, na kwa sasa hivi uchunguzi unaendelea kubaini alivyopata silaha alizokuwa nazo wakati alishikwa na maafisa wa polisi,” alisema kamishna huyo.
Mshukiwa huyo kwa majina Salim Islam alitiwa mbaroni Jumatano na maafisa wa polisi na alipatikana na silaha hatari aina ya bunduki sita, na vifaa vingine vya kutekelezea uhalifu.
Hizi ni baadhi ya juhudi za kamishna huyo wa kaunti kupigana na uhalifu, na kunaswa kwa mshukiwa huyo kunawadia siku chache tu baada ya Marwa kutoa picha ya mshukiwa mwengine ambaye anatafutwa na idara ya polisi kwenye Kaunti hiyo kuhusiana na uhalifu na kuhangaisha wakazi katika kaunti.