Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa ametoa picha ya mshukiwa ambaye anasema kuwa anajihusisha kuendeleza uhalifu na kuwahonga maafisa wa polisi ili kuwaachilia wahalifu kutoka vituo vya polisi.

Marwa amesema kuwa mshukiwa huyo, kwa majina Omar Babs amekuwa mmoja wa vijana ambaye amekuwa katika harakati za kusajili makundi ya uhalifu na pia ni mhusika mkubwa katika visa vingi vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikitekelezwa na makundi hayo.

“Mshukiwa huyu kwenye picha amekuwa akiwahonga maafisa wa polisi ili kuwaachilia wahalifu, na pia anawasajili vijana kuingia katika makundi ya uhalifu, tutamtafuta na wengine ambao wanafanya uhalifu,” alionya kamishna Marwa.

Marwa, katika hutuba na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, alisema kuwa ametoa agizo kwa idara ya usalama kuharakisha msako wa vijana wote pamoja na makundi ambayo yamekuwa katika orodha ya uhalifu kwenye orodha za idara ya polisi.

Marwa alitoa mfano wa kundi moja ambalo alisema linajiita 'Wakali Kwanza', ambalo mara nyingi limehusishwa na matendo ya kihalifu, na kuonya makundi yoyote ambayo yana nia ya kujiunga na makundi haramu kuwa sheria itawandamana vikali.

Hii ni mojawapo ya juhudi kutoka kwa kamishna huyo kujaribu kupigana na uhalifu na uundwaji wa makundi haramu ambayo yamekuwa yakilaumiwa kwa uhalifu katika mji huo wa kitalii.