Mshirikishi mkuu wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa amewaonya maafisa wa trafiki wenye tabia ya kuchukua hongo kutoka kwa wenye magari kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria iwapo watapatikana na hatia.
Akizungumza katika eneon la Matsangoni mjini Kilifi siku ya Alhamisi, Marwa alisema kuwa tayari amepata malalamishi kutoka kwa wahudumu wa magari kuhusu visa vya ulaji rushwa miongoni mwa maafisa wa trafiki Mkoani humo, na sasa anapanga kuuanzisha msako wa kuwanasa.
‘’Nitatumia gari isiyo ya serikali katika harakati zangu za kuwanasa, atakayepatikana atajilaumu mwenyewe,’’ alisema Marwa.
Marwa aidha amewataka wakuu wa idara ya trafiki katika kaunti zote za Pwani kuchunguza mienendo na kuweka rekodi ya maafisa wanaohudumu barabarani, hatua anayosema itasaidia kuwatambua wanaoshiriki ulaji rushwa.
Ni mapema mwaka huu ambapo wachuuzi mjini Mombasa walilalamikia na hata kutishia kugoma, kwa kile walikitaja kama kuchoshwa na maafisa wa mji wanaodai kuwalazimu kutoa hongo huku wengine wakichukua bidhaa zao wanaposhindwa kutoa rushwa.