Kufuatia kijana ambaye alikuwa anatafutwa sana na idara ya polisi katika Kaunti ya Mombasa kujisalmisha, Kamisha wa Kaunti ya Mombasa amewataka wazazi pamoja na wakazi kutoa ripoti kuhusiana na watoto ambao wanawashuku kuwa wanajihusisha na mambo ya uhalifu na ugaidi kwa jumla.
Nelson Marwa, ambaye alihutubia waandishi wa habari katika jiji la Mombasa aliwataka wakazi na wazazi kuchukua nafasi yao na kuboresha usalama wa eneo hilo kwa kuiga mfano wa mzazi wa Mahamoud Mohammed, ambaye alijisalimisha kwenye kituo cha polisi katika wilaya ya Malindi kupitia kwa mwito wa babake.
Kamishana huyo amesema kuwa sharti kila mzazi awajibikie mwanake na kuhakikisha kuwa wanawaongoza watoto wao kwa njia mwafaka, na kusisitiza kuwa idara ya polisi itaendelea kushirikiana na umma kutoa habari muhimu za kuwanasa magenge ya kihalifu ambayo yamekuwa yakiwahangaisha wakazi wa meneo ya Kisauni, Majengo pamoja na Old Town.
“Namshukuru sana baba ya kijana huyo ambaye alijisalimisha kwenye kituo cha polisi cha Malindi na ni hatua nzuri, na bado tutaendelea kuwatafuta washukiwa wengine ambao wamekuwa na rekodi ya uhalifu katika Kaunti hii,” alisema Marwa.
Hii ni hatua nyingine ambayo imechukuliwa huku rais Uhuru Kenyatta akiahidi wakazi kuwa serikali yake itaendelea kuimarisha masuala ya usalama ambao umekuwa na zogo kubwa katika maeneo yote ya Pwani na ambapo sasa anaendelea kuzuru.